BWANA YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Usikubali kuwa mwepesi kusema kwenye kila jambo maana mengine unayojinenea sasa yanaweza kuja kukutesa baadae.
Zaburi 34:13 ''Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila.''
Kinywa chako kinaweza kuzalisha jambo baya au jambo jema kulingana na unavyojitamkia.
Mithali 18:21 ''Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.''
Mfano ulisema kwamba katika ukoo wenu mtu akimaliza tu La saba anaolewa au kuoa hivyo na wewe ukimaliza tu La saba utaoa/ kuolewa. Baadae umefika La saba ukafaulu na kiu ya kusoma ikaja. Unaweza ukasoma Kwa shida maana ulijinenea Kuwa ukimaliza tu La saba unaoa/ kuolewa.
Usikubali kujinenea mabaya maana mengine yanaweza kuja kukutesa baadae.
Hakikisha unajinenea mema sio mabaya.
Mithali 15:2 ''Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri; Bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu.''
Je, Kinywa chako kinatamka maarifa mazuri au kinatamka upumbavu?
Kama kinywa chako kinatamka maarifa mema hakika utavuna matunda yake mema.
Kama kinywa chako kinatamka upumbavu au mambo mabaya hakaika hayo yanaweza kuja kukutesa baadae kama hutaomba rehema na kuyafuta kwa damu ya YESU KRISTO.
Kinywa huwa kinaumba.
Kinywa kinaumba yale unayoyatamka.
Je unatamka nini kwa kinywa chako?
Hata wanaokulaani, hukulaani kwa kinywa hivyo kama unajinenea mabaya na wewe ndio hali itakuwa mbaya zaidi.
Kama kuna watu wanakutamkia mabaya hakikisha unafuta maneno yao kwa damu ya YESU na kwa jina la YESU KRISTO kupitia maombi.
Haribu kila mipango ya kinywa kinachokunenea mabaya,
Kataa kusudi hilo la giza.
Mithali 15:4 '' Ulimi safi ni mti wa uzima; Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo. ''
Huwezi kusema kitu mdomoni kama kama kitu kicho hakiko moyoni mwako.
Ukimuona baba na ndevu zake anadanganya vibinti vidogo Kwa mdomo wake ujue moyo wake huyo baba umejaa uongo na machukizo, Tena moyoni wake jini mahaba ameweka kigoda na kukaa.
Na kabinti kanakodanganywa na kakakubali Kwa mdomo hako nako moyoni kumejaa dhambi na vitamaa vya kishetani.
Kama moyoni mwako umemjaza shetani hakika kinywa chako kitaonyesha ushetani.
Mithali 12:20 '' Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu; Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha.''
Ukijaza moyoni utakatifu hakika kinywa chako kitathibitisha.
kile kilichomjaa mtu moyoni ndo kimtokacho mdomoni!!
Moyo ukijaa matusi, mdomoni utanena matusi tu kila wakati.
kuna baadhi ya watu hawawezi kuongea bila kutukana tusi lolote. Na walio wengi sasa hivi kutukana imekua kama fasheni.
Tumeambiwa kila neno baya tunalotamka mdomoni tutamtoa hesabu yake siku ya mwisho, kama hututafuta maneno hayo sasa kwa kutubu.
Warumi 3:12-14 ''Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira i chini ya midomo yao. Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.''
Maneno ya watu hutumika katika mambo mema.
Maneno ya watumishi wa MUNGU yana maana sana ila angalizo kwa watumishi ni hili;
Maneno ya mtumishi Wa MUNGU yanatakiwa yawe maneno ya kuwaponya watu na sio kuwaua.
Maneno ya kuwaponya watu wakati mwingine yanaweza kuwa Makali na ya makaripio makali sana na ya kuonya na kukemea Kwa ukali sana maana huko ndiko kuwaponya watu.
Mtumishi anayekutia moyo kwenye dhambi yako Huyo anakuua wala hakuponyi.
Mtumishi anayekukemea huyo anakuponya.
Kwa mtumishi wa KRISTO kunatakiwa litoke Neno la kuponya na sio kuua.
Najua kila aliyeokolewa na BWANA YESU huyo ni mtumishi Wa KRISTO hivyo ni muhimu sana wote tuwe na maneno ya kuponya na sio kuua.
Matendo 4:31 '' Hata walipokwisha kumwomba MUNGU, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa ROHO MTAKATIFU, wakanena neno la MUNGU kwa ujasiri. ''
MUNGU anauangalia utakatifu wako siku hadi siku.
Hivyo ni muhimu kuongeza utakatifu na sio kuupunguza utakatifu au kuufuta kabisa utakatifu.
Ukidumu katika utakatifu hiyo ni Kwa faida yako peke yako na sio mtu mwingine yoyote.
Kinywa ni muhimu sana katika kukamilisha utakatifu wako.
Kuna watu wameokoka miili ila vinywa vyao havijaokoka kabisa maana hutamka matusi kila siku.
Utakatifu ambao mteule anauonyesha kanisani inatakiwa utakatifu huo huo auonyeshe nje ya jengo la kanisani.
Maisha ya kuigiza ni Kwa uangamivu Wa muigizaji mwenyewe.
''Wana wetu na wawe kama miche Waliokua ujanani. Binti zetu kama nguzo za pembeni Zilizonakishwa kwa kupamba hekalu. -Zaburi 144:12''
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili
0 comments:
Post a Comment