Sunday, May 1, 2016

MAMBO SABA(7) YA KUFANYA WANANDOA ILI WAIFANYE NDOA YAO IWE KIELELEZO.



BWANA YESU atukuzwe mpendwa.
Karibu nikujuze Neno la MUNGU.
Leo nazungumzia ndoa takatifu.
Ndoa ni makubaliano rasmi matakatifu kati ya Mwanaume na Mwanamke kuishi pamoja kama mke na mume, kwa kuanza na utakatifu na kumaliza wakiwa watakatifu.
Ndoa takatifu ni kati ya Mwanaume mtakatifu na Mwanamke mtakatifu watakapoamua kufunga ndoa takatifu katika MUNGU aliye Mtakatifu.
MUNGU anasema;
'' Kwa hiyo mtayashika maagizo yangu, na kuyafanya; mimi ndimi BWANA.-Walawi 22:31''
Ndoa ni agano takatifu la siku zote za kuishi kwa wawili hao.
Ndoa takatifu inatakiwa iambatane na utakatifu.
Ndoa takatifu inaanza na Wokovu wa BWANA YESU na kuishi kwa kulitii Neno la MUNGU.
Yakobo 4:7 ''Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.''
Kuna ndoa zilianzia bar, wanandoa hao wanatakiwa watubu na kuanza kuishi maisha matakatifu ya wokovu wa BWANA YESU.
Kuna ndoa zilianzia vichakani, wanandoa hao wanatakiwa watubu na kuanza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa BWANA YESU.
Ndoa ili iwe takatifu ni lazima iambatane na utakatifu wa wanandoa husika.
Kuna ndoa ni vielelezo vizuri kwa wengine lakini kuna ndoa ni vielelezo vibaya kwa ambao wanataka kuingia katika ndoa.
Ndoa kuwa kielelezo ni kuwa ndoa ya mfano unaotakiwa kuigwa.
Ndoa ni takatifu sana hivyo inatakiwa iwe baraka na sio balaa.
Waefeso 5:31 '' Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.''
Ili wanandoa waifanye ndoa yao iwe kielelezo Chema kwa wengine inabidi wafanye yafuatayo;
1. Inabidi wanandoa kila mmoja kuiheshimu ndoa.
Waebrania 13:4-5 ''Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu. Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.''
-Anayeiheshimu ndoa yake hataisaliti kwa vyovyote na kwa lolote.
-Anayeiheshimu ndoa yake atavumulia hata kama uchumi hauko sawa kwa wakati huo.
-Anayeiheshimu ndoa yake hatalaghaiwa na pesa ili aisaliti ndoa yake.
-Anayeiheshimu ndoa yake ataiombea ndoa yake maana ahadi ya MUNGU ni kwamba hatawapungukia.

2. Kila mwanandoa kuwa huru ndani ya ndoa.
Wagalatia 5:13 ''Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo.''
-Wanandoa wakristo wamewekwa huru mbali na dhambi na tena kwa sababu wako huru basi sio watumwa wa dhambi.
Mwanandoa kuwa huru maana yake ni yule anayeutumia uhuru wake vizuri, kwanza kwa kumhofu MUNGU na pili kwa sababu anautaka uzima wa milele.
Uhuru mwingine kwenye ndoa ni uhuru wa haki katika ndoa.
Lazima mama awe na uhuru kwenye ndoa yake na baba awe na uhuru kwenye ndoa yake.
Wagalatia 5:1 ''Katika ungwana huo KRISTO alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa.''
Hakuna haja ya mama hadi amsubiri baba aje atoe kibali ndipo siku hiyo familia wale wali.
Hakuna haja ya baba kuchelewa kidogo tu kazini basi tendo la ndoa linafutwa kwa mwezi mzima.
Kama wanandoa wanaojitambua inabidi kwanza kila mmoja awe na uhuru kwenye ndoa yake. Kushauriana ni muhimu sana lakini isiwe utumwa kwenye ndoa.
Mama asiwe mtumwa na baba asiwe mtumwa katika ndoa bali wote wawe huru wakimpendeza kwanza MUNGU kisha ndoa yao.
Warumi 6:22 '' Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa MUNGU, mnayo faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele.''

3. Kila mwanandoa kuishi maisha matakatifu.
1 Petro 1:15 ''bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;''
-Maisha matakatifu kwa wanandoa ni mtaji wao wa kuifanya ndoa yao iwe kielelezo kwa watu walio nje.
-Maisha matakatifu kwa wanandoa ni kinga yao ya kuifanya ndoa yao isishambuliwe na adui.
-Maisha matakatifu ni mwanga wa kuwamulikia wanadoa katika njia yao ya maisha yote ya duniani.
Maisha matakatifu ndilo jambo muhimu zaidi kwa kila mwanadamu akiwemo mwanandoa katika maisha yote ya duniani.

4. Kila mwanandoa kumuona mwenzi wake kuwa ni bora kuliko nafsi yake.
Wafilipi 2:3-4 ''Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.''
-Mke akimuona mume wake ni bora kuliko nafsi yake na mume naye akamuona mke wake ni bora kuliko nafsi yake hakika ndoa hiyo itakuwa kielelezo chema mbele ya jamii.
-Kumuona mwenzako ni bora kuliko nafsi yako ni kuifanya ndoa yenu kuwa na afya njema ya kuwafanya muishi kwa amani muda mrefu sana.
-Mume akiwa anamjali zaidi mkewe badala ya kujijali yeye hakika ataleta furaha kwa mke na kuleta furaha kwenye ndoa.
-Mke kama atamjali mumewe na kumuombea daima hakika jambo hilo litaleta baraka kwenye ndoa na amani na furaha kuu.
5. Kila mwanandoa kutii utaratibu mwema waliojiwekea ndani ya ndoa yao.
-Kuna ndoa zimejiwekea utaratibu mzuri katika ndoa yao.
Kuna ndoa zimejiwekea hata utaratibu wa kukutana kimwili, kusaidia wazazi, kutembelea ndugu, kufunga na kuomba.
Ni vizuri pia kama kila mhusika ataufuata utaratibu waliojiwekea wenyewe kwa furaha zao.
Kama ndoa yenu mmejiwekea taratibu mbalimbali ni vizuri sana kujulishana kama mmoja anataka kufanya tofauti au kama kuna dharula.
Kama wanandoa mnaomcha MUNGU mtajiwekea utararibu au mipango ya muda fulani basi ni muhimu sana mkamhusisha na MUNGU katika mipango yenu ili awafanikishe.
Baada ya kuipanga mipango hiyo mnatakiwa kila mmoja wenu aiheshimu ili mtafaruku wowote usitokee.
Kufanya hivyo ni kuifanya ndoa kuwa kielelezo maana majirani hawatasikia hata siku moja mkizozana baada ya mmoja wenu kuvunja utaratibu.
Ni muhimu mkawa na mawasiliano ya mara kwa mara na kujulishana katika yote kwa upendo na amani ya KRISTO.
Wakolosai 3:14-15 ''Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. Na amani ya KRISTO iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani''
6. Kila mwanandoa kuzingatia usafi wa mwili na roho
2 Kor 7:1 ''Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha MUNGU.''
-Ni muhimu sana kila mwanadoa kuwa msafi wa mwili na roho.
Usafi wa mwili ni usafi wa mwili na kila unachovaa katika mwili.
Usafi wa roho ni kuishi maisha matakatifu.
Ni muhimu sana kuwa watakatifu.
Uchafu kwa mmoja wa wanandoa unaweza kuleta kero kwa mwenzi wake.
Kila mtu anajua usafi ni nini hivyo ni muhimu sana kuwa wasafi wa mwili na roho.
7. Kila mwanandoa kuhakikisha ndani ya ndoa yao KRISTO ni yote katika wote.
Warumi 8:10-14 ''Na KRISTO akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki. Lakini, ikiwa ROHO yake yeye aliyemfufua YESU katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua KRISTO YESU katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa ROHO wake anayekaa ndani yenu. Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili, kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa ROHO, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU''
-KRISTO ni pekee wa uzima wa milele.
Huwezi ukautaka uzima wa milele harafu humtaki KRISTO.
Mwanandoa makini ni yule anayemtii KRISTO na Neno lake.
Msingi wa ndoa yenu unatakiwa uwe BWANA YESU.
Kuishi kwa ndoa yenu kunatakiwa kuwe kwa utukufu wa MUNGU.
Ndoa yenu inatakiwa iwahubirie wengine uzuri wa WOKOVU.
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

0 comments:

Post a Comment