Sunday, May 1, 2016

AU HAMJUI?



BWANA YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Neno la MUNGU la leo linamtaka kila mwanadamu kujua, kuchukua hatua na kubadilika katika mfumo wake wa maisha.
Au hamjui?
''Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi-1 Kor 6:9-10''
Katika ambao hawataurithi ufalme wa MUNGU ni pamoja na Waasherati, waabudu sanamu, wazinzi, wafiraji, walawiti, wezi, watamanio, walevi, watukanaji na wanyang'anyi.
Watenda dhambi wote hawataurithi uzima wa milele kama hawatatubu kipindi hiki wakiwa hai duniani.
Anayesamehe dhambi ni BWANA YESU pekee hivyo kama kuna mtu pia hamwitaji YESU basi huyo ndugu hauhitaji uzima wa milele.
Biblia inataka kila mwanadamu ajue hivyo ili aamue kama anautaka uzima wa milele au hautaki.
Kuna watu inawezekana kabisa wao sio waasherati lakini ni waabudu sanamu, hao wasipotubu wakati huu wakiwa hai hawawezi kuurithi ufalme wa MUNGU.
Kuna watu sio waabudu sanamu lakini ni wazinzi, hao hawataurithi ufalme wa MUNGU wasipotubu wakati huu wakiwa hai.
Kuna watu inawezekana kabisa sio wazinzi wala hawajawahi kutoka katika ndoa zao lakini tatizo lao hufanya mapenzi kinyume na maumbile, Biblia inawaita wafiraji, hao nao wasipotubu sasa wakiwa hai hakika uzima wa milele hauwahusu.
Ndugu mmoja anasema ''mradi sitoki nje ya ndoa'' lakini huyo huyo hufanya mapenzi kinyume na maumbile na kujivunia kilo nyingi za dhambi kila siku maana uovu huo ni mbaya sana na una madhara mengi sana kiroho na kimwili.
Kwa sababu Biblia kwa ukali kabisa imelitumia hilo neno ''wafiraji''
basi ngoja na mimi nilitumie ili kusema ukweli huu kwamba hakuna mbingu ya watu waliokuwa wafiraji.
Wewe mume unayemfira mke wako, huo ni uovu mkuu, tubu na acha uovu huo maana unapotenda hayo naomba utambue pia kwamba usipotubu kuna jehanamu inawangoja wafiraji wote. ukitubu leo na kuacha dhambi hakika unasamehewa.
Mathayo 3:2 ''Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. ''
Wewe mke unayekubali kufirwa, huo ni uovu mkuu na kama usipoacha kuingiliwa huko kinyume na maumbie kuna ziwa la moto linalowangoja wafirwaji. tubu na acha uovu huo, kama unadhani huo ni upendo basi huo ni upendo wa kishetani, ni kamba ya kukuvuta taratibu hadi jehanamu. tubu na geuka leo maana watenda dhambi hawana nafasi katika ufalme wa MUNGU. Lakini ukitubu leo na kuokoka na kuacha uovu huo utapona.
ufiraji kama ulivyo ulawiti ni uovu mkuu na Biblia iko wazi ikisema kwamba watendao uovu huo hawataenda uzima wa milele. Dawa ni kutubu, kuacha uovu huo na kuanza kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
kuna watu huwalawiti hata watoto wao wa kiume na wa kike.
Kuna vijana hulawitiwa.
Kuna watu huwalawiti hadi watoto wadogo.
Kuna watu hulawiti hadi wanyama.
Huo ni uovu mkuu na Biblia iko wazi sana ikisema;
''katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa MUNGU.-Wagalatia 5:21''
Inawezekana kabisa kuna watu sio wazinzi lakini wao ni walevu, huiona dhambi ya ulevi ni ndogo lakini Biblia iko wazi sana hapo juu kwenye andiko la kwanza ikisema walevi hawataurithi ufalme wa MUNGU.
''Kunywa kidogo ila usilewe'' ni ajenda ya shetani iliyowekewa muhuri na baadhi ya viongozi wa kanisa wasioipenda mbingu.
Je hamjui?
2 Kor 6:14 ''Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? ''
Nuru ni wokovu na kuishi katika utakatifu kama Biblia inavyoelekeza.
Giza ni shetani na mambo yake yote.
Watu wa MUNGU wanaotarajia uzima wa milele hawatakiwi kujichanganya na mambo ya giza katika maisha yao.
kuna watu kwa waganga wanaenda na kanisani wanaenda, huo ni upagani hata kama kanisani uko kila wiki.
acha mambo ya giza na dumu katika kanisa ukidumu pia katika kulitii Neno la MUNGU.
Siku hizi kuna mashoga hadi kanisani. ni machukizo na Biblia iko wazi sana ikisema kwamba hakuna mbingu ya washoga. ndoa za mashoga ni ndoa zenye agano la shetani, ni ndoa ambazo machozi ya furaha hayatoki wakati wa kufunga ndoa lakini machozi ya huzuni yanaweza kutoka kwa kila mtenda dhambi hiyo kama ndoa hiyo itadumu hadi kifo maana baada ya kifo cha mwenye dhambi kuna ziwa la moto baadae.
Biblia iko wazi kabisa kukataza ushoga.
Kuna matukio mawili yaliwahi kunishangaza sana baada ya kuyasikia. tukioa la kwanza kuna kwaya moja, mmoja wa waimbaji mahiri sana wa kiume kwenye kwaya hiyo ni shoga. sikuamini lakini mmoja wa waimbaji wa kwaya hiyo ndiye aliyeniambia huku akidai yeye mwenyewe aliwahi kutakwa na yule shoga, akakataa na kumkemea na kumripoti kwa mchungaji wa kanisa. baadae ilikuja kuwa wazi juu ya mwimbaji huyo mwenye kipaji na tegemeo katika kwaya hiyo. ni hatari sana. hilo ni giza katikani ya nuru.
Hakutakiwi kuwapo mtu wa hivyo katika kundi la wateule wa MUNGU. Ni machukizo makuu hayo na Biblia iko wazi ikisema hakuna uzima wa milele kwa mashoga yaani kwa wanaume wanaofirwa na wanaofira.
Siku moja pia kuna mtumishi mmoja alishuhudia mbele ya kanisa mahali fulani juu ya tabia ya mume wake kumwingilia kinyume na maumbile kila siku. kwa jinsi ndugu yule alivyokuwa amesimama kiroho nilitamani kulia.
Ni hatari sana kuolewa na mtu asiye na hofu ya MUNGU.
Ni hatari sana kuoa mwanamke mpagani.
Ukiwa na mwenzi wa ndoa mwenye tabia hiyo ni heri kuachana naye kabisa, maana heri upate uzima wa milele kuliko kupata jehanamu iliyozaliwa na ndoa.
Hakutakiwi kuwepo giza katika nuru.
1 Yohana 1:5-7 '' Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba MUNGU ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake.Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. ''
Giza ni giza na nuru ni Nuru, ni heri kuikimbilia Nuru ambayo ni BWANA YESU.
Au hamjui?
2 Kor 6:16 ''Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la MUNGU na sanamu? ''
Sanamu leo zinaabudiwa kwenye baadhi ya nyumba za ibada..
Sanamu leo imegeuka Mungu kwa baadhi ya watu.
Biblia iko wazi sana ikisema kwamba hakuna mapatano kati ya sanamu na kanisa la MUNGU.
Kwenda kwa waganga wa kienyeji ni kuabudu sanamu.
Kumwabudu Mariamu ni kuabudu sanamu.
Biblia iko wazi ikisema
''Basi, kwa kuwa sisi tu wazao wa MUNGU, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu. -Matendo 17:29 ''
MUNGU hayuko katika sanamu yeyote bali MUNGU yuko mbinguni.
BWANA YESU hayuko katika sanamu ya aina yeyote bali BWANA YESU yuko mbinguni.
Watakatifu wa zamani hawako katika sanamu yeyote bali wako mji mtakatifu wakifurahi kwa BWANA YESU.
Mwanadamu kujiita Mungu ni kujitengeneza mwenyewe awe sanamu na aabudiwe.
Ni uovu mkuu sana.
Biblia iko wazi sana ikisema
Zaburi 29:2 ''Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu.''
Kuna watu badala ya kumpa MUNGU heshima wao huzipa heshima sanamu zilizotengenezwa na wanadamu.
Tangu miaka yote katika Biblia MUNGU aliwaambiwa watu wake wavunje sanamu zote zinazoabudiwa na kunyenyekewa na wanadamu.
Tangu zamani MUNGU amekataza watu wake wasihesimu sanamu.
Kumb 7:5 ''Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga. ''
Je hamjui?
1 Kor 6:15 ''Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya KRISTO? Basi nivitwae viungo vya KRISTO na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha!''
Tena, Je Hamjui?
1 Kor 6:16 '' Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? ''
Je Hamjui?
1 Kor 6:19 ''Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la ROHO MTAKATIFU aliye ndani yenu, mliyepewa na MUNGU? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;''
Mkristo aliyeokolewa na BWANA YESU huyo ni hekalu ya ROHO MTAKATIFU.
Huyo ni makazi ya ROHO wa MUNGU.
Kama mkristo huyo akianza dhambi ROHO wa MUNGU huondoka ndani yake, ni hatari sana ROHO wa MUNGU kuondoka katika maisha ya Mkristo.
Kanisa ni mwili wa KRISTO na kanisa na wakristo wote wanaomtii KRISTO YESU.
Kuna watu wameungwa na kahaba.
Hawa ni wale watenda dhambi, hao wameungwa na dhambi yaani wao na dhambi ni mwili mmoja hadi watakapotubu ndipo watatengwa na dhambi hizo.
Kama wewe unajiita Mkristo kisha humtii KRISTO hakika wewe hauna sehemu katika ufalme wake KRISTO. Tubu na rejea ili usamehewe.
Matendo 3:19 ''Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA; ''
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

1 comment: