Sunday, May 1, 2016

SIKU YA MWISHO SIRI HAZITAKUWA SIRI TENA.



BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Siku ya mwisho mambo yote yatakuwa peupe.
Isaya 13:9-11 '' Tazama, siku ya BWANA inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake. Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze. Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali;''
Kazi moja kubwa itakayofanyika siku ya mwisho ni hukumu.
Hukumu hiyo itafanywa na BWANA YESU na siku hiyo kutakuwa na makundi mawili tu ya wanadamu; Kundi la kwanza ni watu wanaoenda uzima wa milele na kundi la pili ni watu wanaoenda jehanamu.
Siku hiyo hakutakuwa na siri tena.
Waabuduo halisi watajulikana siku hiyo.
Wanao igiza utakatifu wataonekana siku hiyo.
Wanaotumainia dini siku hiyo itajaulikana wazi.
Mambo ya siri yaliyofanywa na kila mwanadamu yote yatakuwa peupe.
Walioishi maisha safi ya wokovu wa BWANA YESU wataenda uzima wa milele.
Waliomkataa BWANA YESU siku hiyo wataenda jehanamu hata kama walitenda baadhi ya matendo mema, ila kumkataa tu BWANA YESU hapo watakuwa wameukataa uzima wa milele.
2 Petro 3:10-12 '' Lakini siku ya BWANA itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, mkitazamia hata ije siku ile ya MUNGU, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? ''

Ni siku ya furaha kwa waliookoka kisha kuishi maisha matakatifu na ni siku ya kujuta na kulia kwa walioukataa wokovu wa BWANA YESU.
Kila kitu kitakuwa wazi kabisa.
Mwanamke aliyekuwa anaisaliti ndoa yake kwa usiri mkubwa siku hiyo itajulikana hadharani kwamba yeye ulikuwa msaliti.
Wewe baba ambaye una nyumba ndogo siku hiyo itajulikana wazi dhambi yako hiyo.
Wewe mfanyakazi wa serikali unayeiba pesa siku hiyo wizi wako utajulikana.
Wewe mchawi unayeroga watu kwa siri huku ukienda kanisani kama kujificha uovu wako huo watu wasijue siku hiyo dhambi yako hiyo itajulikana.
Wewe unayetapeli watu siku hiyo mambo yako yote yatakuwa peupe.
Wewe changudoa siku ya mwisho mambo yako yote yatakuwa peupe.
Biblia inaonya sasa ili mwenye sikio la kusikia aache dhambi na kutubu na kuokoka.
1 Petro 3:10-11 ''Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana. ''
Ndugu, je umelielewa andiko hilo?
Ni maonyo na maagizo muhimu kutoka kwa MUNGU aliye hai, akikuonya kwamba uache mabaya na utende mema.

Wewe ambaye huwa unafanya uovu kwa kumuogopa tu mchungaji, mchungaji akiwa karibu wewe ni mwema sana lakini mchungjai akiwa mbali unafanya dhambi, ndugu siku hiyo mambo yake yote yatakuwa peupe.
Wewe uliye na utajiri wa kishetani siku hiyo ya mwisho itajulikana.
Wewe unayetembea na hirizi siku hiyo mambo yako yote yatakuwa peupe na dhambi yako hiyo itakuwa dhahili.
Hakuna mwanadamu ambaye atasema ameonewa maana hukumu ya MUNGU iko wazi sana maana hata matendo yako mabaya yatazungumza.
Biblia inasema hivi kuhusu hiyo siku ya hukumu.
Ufunuo 20-12 ''Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.''
Ni siku ya kutisha, ni siku ambayo wanaojivunia kazi zao na utajiri wao havitawasaidia.
Kuna watu leo kila wakiambiwa waende kanisani wanasema wako busy kazini, lakini siku hiyo hakuna mwanadamu hata mmoja ambaye atalipwa kulingana na kazi yake serikalini, bali atalipwa sawasawa na matendo yake.
Ni siku ya mambo yote Peupe.
Lakini pia iko furaha kubwa kwa watakatifu wa MUNGU waliosafishwa kwa damu ya YESU KRISTO.
Hatutakiwi tuishi kwa sababu tu tunaishi bali tunatakiwa tuishe kwa sababu KRISTO YESU anaishi ndani yetu.
Tuishi maisha matakatifu siku zote.
BWANA YESU anasema;
'' Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za BABA yangu, na mbele ya malaika zake.Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.- Ufunuo 3:5-6 ''

Ndugu yangu, nakuomba futa utaratibu wako wa dhambi na anza kuishi maisha matakatifu ukiwa umeokoka.
Nakuomba katika maisha yako ufunge ukurasa wa dhambi kuanzia leo na fungulia ukurasa wa matendo mema kuanzia leo.
Sio lazima mawazo yako ya jana yawe ndio mawazo yako ya leo.
Kama jana uliwaza dhambi naomba leo uwaze kuokoka na utakatifu.
Okoka kisha ishi maisha matakatifu.
Kuendeleza mawazo ya jana yasiyokusaidia ni kujipoteza huku unajiona.
Matendo 3:19 ''Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;''

✔Kumjua YESU KRISTO ni kuijua njia ya uzima wa milele.
✔Kumkataa YESU KRISTO ni kuukataa uzima wa milele
''Angalieni msimkatae yeye anenaye. Maana ikiwa hawakuokoka wale waliomkataa yeye aliyewaonya juu ya nchi, zaidi sana hatutaokoka sisi tukijiepusha na yeye atuonyaye kutoka mbinguni; ambaye sauti yake iliitetemesha nchi wakati ule; lakini sasa ameahidi akisema, Mara moja tena nitatetemesha si nchi tu, bali na mbingu pia.- Waebrania 12:25-26
Ndugu zangu ni muhimu sana kuanza kuishi maisha matakatifu.
Kama umeokoka hakika naomba utambue kwamba tumeokolewa na BWANA YESU ili tuishi maisha matakatifu.
Kama hujaokoka hakika nakuomba uokoke, kumbuka dunia na mambo yake yote yatapita.
Kama kuna dhambi unadhani huwezi kuicha nakuomba Kimbilia maombezi na uwe muwazi kujieleza mbele ya wachungaji, maana kufanya siri haitakusaidia bali kusema ukweli na kuhitaji maombezi utapona.
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

0 comments:

Post a Comment